KWA NINI NDOA HAZIDUMU
· Je, Kuna Haja ya Kuhuisha Mafunzo ya Jando na Unyago?
· Dar Peke Yake Kuna Wastani wa Ndoa 360 Zinavunjika Kila Mwezi.
· Kuongezeka kwa Tabia za Ushoga Katika Jamii.
Hivi karibuni, tumemsikia
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii akisema kuwa kuna
haja ya kuchukua hatua na kutafuta kwa kina chanzo cha kuvunjika kwa ndoa
nyingi nchini.
Mwenyekiti huyo wa Kamati ya
Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, ndugu Stanslaus Nyongo, aliyasema hayo
siku ya Jumatatu mwezi wa Septemba tarehe 5, 2022 baada ya kukutana na wizara
ya maendeleo ya jamii, jinsia na makundi Maalum.
Dar es Salaam pekee yake zaidi ya
ndoa 360 kwa mwezi zinavunjika, ni wastani wa ndoa 12 zinafunjika kila siku.
Hili linaweza kuwa linachangiwa
na sababu nyingi kutoka kwa wanandoa wenyewe. Lakini kuna vitu ambavyo
tukiviangalia tunajua kuwa ni moja ya sababu zinazopelekea ndoa na mahusiano
mengi kuweza kuvunjika.
Wanandoa wengi sasa hivi
wanashindwa kuishi maisha ya ndoa, wengi wao wamekuwa wanaharakati zaidi katika
ndoa kuliko kuwa walezi, hali ambayo imesababisha migogoro na kuvunjika kwa
ndoa nyingi, jambo hili linaathiri ustawi wa familia, maisha, ufanisi katika
utendaji kazi.
Watu wengi wanaingia katika ndoa
bila kupata elimu na mafunzo ya kutosha kuhusu maisha ya ndoa, haswa kwa
kupotea kwa mafundisho ya kijadi ya Jando na Unyago kwa wavulana na wasichana
waliobaleheka.
Watu wengi wanaishi kwenye ndoa
au mahusiano kusogeza tu siku, ilimradi kunakucha. Ndoa nyingi kwa sasa
zimekosa ushirikiano katika kutoa maamuzi ya pamoja yatakayoweza kuwasaidia
kujenga familia bora na maisha mazuri ya sasa na ya baadaye.
Inashangaza sana kuona watu
wanaoishi pamoja kila mmoja ana mipango na mikakati ya maisha yake. Huyu
anawaza kufanya hivi, yule anawaza kufanya vingine na awaambiani. Hakuna
ushirikiano wowote kama wanandoa wa kuweza kukaa chini na kushirikishana
malengo mbalimbali yatakayoweza kuwasaidia katika kujenga na kuboresha maisha yao.
Sababu kubwa nyingine
zilizotolewa kutoka kwenye tafiti kadhaa wa kadha kuwa ndio chanzo cha ndoa
nyingi kuvunika na ndoa nyingi ziwe katika foleni ya kuvunjwa, ni Mmonyoko
mkubwa wa maadili na ukatili mkubwa wa kijinsia, hasa kwa watoto ni mkubwa
inahitaji Watanzania wajipange, hili kutokomeza hili tatizo katika jamii zetu.
Chanzo kingine ni katika vingi ni
wivu uliopindukia mipaka, ugumu wa maisha, kuwa na kipato duni, watu kuathirika
kiakili, kulazimisha kuingiliana kinyume na maumbile, baadhi ya wenza kuwa na
tabia za kishoga, kukosa uaminifu na wenza kupelekea kuchepuka nje ya ndoa zao.
Na Ugomvi wa wanandoa unapelekea
watoto kuteseka kwa kukosa malezi bora na hatimaye watoto hao kujikuta
wakifanyiwa ukatili wa kingono kutokana na kutokuwa na malezi mazuri kutoka kwa
wazazi wa pande zote mbili.
Kuna haja sasa ya serikali kufanya utafiti kupitia wizara zake hili kutengeneza mtaala maalum wa mafunzo ya Jando na Unyago na Mizungu ya kimaisha kwa vijana wa shule za Msingi na Sekondari.
Misamiati
· Kuhuisha, (Huisha): Anzisha tena jambo ambalo lililokuwa limesita kuendelea.
· Jando na Unyago: Mafunzo ya nadhria na vitendo yanayohusu malezi kwa wavulana/wasichana kuhusu mila na desturi za jamii zao
· Mizungu: Matendo ya maarifa ya nyanja mbalimbali ya kimaisha na ya busara ndani ya kumbi yanayofunzwa watu kwa siri.
· Kumbi: Mahali panapofanyika shughuli za jando/unyago
0 comments:
Post a Comment
Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?