Thursday, 8 September 2022

 VITA VYA IRELAND YA KASKAZINI
1968–1998

Muungano Jumuishi wa Ufalme wa Uingereza na Scotland, Wales na Ireland ya Kaskazini au United Kingdom, ambao chini ya ugatuzi wa madaraka, nchi washirika zina kiasi fulani cha madaraka ya ndani, uliingia matatizo makubwa mwaka 1968 wakati Wakatoliki wa Ireland ya Kaskazini walipoanzisha mapambano ya silaha ili kujitoa kwenye muungano huo na kutaka kuwa sehemu ya Jamhuri ya Ireland.

Ili kuyaelewa vizuri mazingira ya vita hivi vya wenyewe kwa wenyewe kwenye taifa kubwa na kongwe kama Uingereza, hatuna budi kurejea kwenye historia kwamba kisiwa cha Ireland kilikuwa koloni la Waingereza kuanzia karne ya 13. Ifahamike kwamba sehemu kubwa ya Waingereza ni Waprotestanti wa Kianglikana lakini wakaitawala Ireland yenye idadi kubwa ya Wakatoliki na hivyo kutengeneza mpasuko mkubwa wa kidini.

Baada ya miaka mingi ya kudai uhuru, Uingereza ikakigawa kisiwa hicho kwa msingi wa kulinda maslahi ya Waprotestanti waliokusanyika zaidi Kaskazini Mashariki mwa kisiwa hicho. Hivyo, harakati za kudai uhuru zilipopamba moto miaka ya 1920, Ireland ya Kaskazini ikatangaza kuendelea kuwa sehemu ya ufalme wa Uingereza, hivyo, kuzua mgogoro mpya kati ya Waprotestanti na Wakatoliki katika jimbo hilo, Waprotestanti wakitaka nchi hiyo ibakie kuwa sehemu ya muungano na Wakatoliki wakiukataa muungano huo na kutaka jimbo hilo lirejee kuwa sehemu ya Jamhuri ya Ireland.

Mwaka 1949, kisiwa hicho bila sehemu yake ya kaskazini mashariki (yaani Ireland ya Kaskazini) kikajitangaza kuwa Jamhuri ya Ireland na kujitoa kwenye Jumuiya ya Madola. Uhasama mkubwa ukapamba moto kati ya makundi hayo mawili ndani ya Ireland ya Kaskazini na kusababisha kuanza kwa mapambano ya silaha mwaka 1969.

Vita hivyo vilidumu kwa miaka 30 (1968 – 1998) na kugharimu maisha ya watu 3,600 na wengine 30,000 kujeruhiwa kabla ya kupata muafaka ambao umeipa Ireland ya Kaskazini madaraka ya kujiongoza katika maeneo kadhaa na mfumo wa uongozi shirikishi. Jimbo hilo lina bunge lake lenye mamlaka kwenye maeneo yaliyoainishwa na ambayo Bunge la Uingereza haliyagusi. Vilevile, yapo mamlaka ya utendaji ya pamoja ambapo kuna Waziri Kiongozi na Naibu wake wenye mamlaka sawa na wanatoka makundi makubwa mawili yaliyohasimiana kwa miaka mingi jimboni humo.


0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!