Thursday, 8 September 2022

 
MCHANGO WA TANZANIA KATIKA UKOMBOZI WA AFRIKA

Tanzania imekuwa mstari wa mbele kutetea masuala yahusuyo haki za binadamu duniani, kuunga mkono juhudi za ujenzi wa demokrasia na misingi yake sambamba na utawala bora pamoja na kuhamasisha Umajumui wa Afrika.

Tanzania ni miongoni mwa nchi tano zilizokuwa Mstari wa Mbele wa Mapambano katika kuhakikisha kuwa nchi za Afrika zinapata uhuru wake kutoka katika makucha ya wakoloni na ilikuwa tayari hata kuchelewesha uhuru wake ili nchi nyingine za Afrika zijinasue kutoka kwenye mikono ya wakoloni.

Katika kufanikisha hilo Tanzania ilishirikiana na Angola, Botswana, Msumbiji na Zambia ili kufikia azma ya pamoja ya kulikomboa Bara la Afrika na hasa nchi za Kusini mwa Afrika sambamba na kupinga ubaguzi uliokuwa ukifanywa na Makaburu katika nchi ya Afrika Kusini.

Nchi hizi pia zilipambana kusaidia kuuondoa utawala wa wachache katika nchi za Afrika Kusini, Namibia na Rhodesia ya Kusini ambayo kwa sasa inatambulika kama Zimbabwe.

Kipekee, Tanzania ilitoa maeneo mbalimbali yaliyotumika kwa mafunzo ya medani na mbinu za kivita. Maafisa na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) walitumika kutoa mafunzo katika vyuo na makambi mbalimbali nchini. Vyuo na Makambi hayo yalikuwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Mbeya, Iringa, Dodoma, Tabora, Tanga, Morogoro, Kagera, Arusha, Mwanza, Singida na Pwani.

Vilevile, Tanzania ilipeleka askari wake kwenda kusaidia majeshi ya ukombozi ya Msumbiji (FRELIMO) kupitia kambi ya kijeshi ya Farm 17 iliyopo Nachingwea mkoani Lindi iliyokuwa ikitumiwa na jeshi hilo la Msumbiji. Askari wengi wa Tanzania walifariki kishujaa katika harakati za kuhakikisha Msumbiji inajikomboa kutoka kwenye utawala dhalimu wa Wareno.

Kati ya mwaka 1973 hadi 1975 Wareno kwa kushirikiana na makaburu wa Afrika Kusini walishambulia mara kwa mara maeneo ya Mtwara na Lindi kwa ndege za kivita na kuua, kujeruhi watu wengi na kuharibu mali na miundombinu mbalimbali. Aidha, Wareno walimwaga sumu iliyoharibu na kuteketeza mashamba ya mkonge mkoani Mtwara wakiamini kuwa kufanya vile kungeyumbisha uchumi wa Tanzania ambao kipindi hicho ulitegemea sana mazao ya pamba na katani. Hayo yote yalifanyika baada ya kuona kuwa Tanzania imekuwa ngome kubwa ya wapiganaji wa FRELIMO.

Kuteketezwa kwa mashamba ya mkonge kuliathiri uchumi wa nchi lakini haikuwavunja moyo Watanzania. Badala yake Tanzania ikaongeza nguvu kuisaidia FRELIMO si katika vita tu bali katika kujenga upya utawala wa kiraia ambao ungekidhi matakwa ya watu wa Msumbiji.

CHUO CHA DIPLOMASIA

Hivyo basi, baada ya Msumbiji kupata uhuru mwaka 1975 Serikali za Tanzania na Msumbiji zilitiliana saini ya makubaliano ya kuanzishwa kwa chuo kilichoitwa Chuo cha Elimu ya Juu kwa Wapigania Ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika ambacho kilianzishwa rasmi Dar es Salaam tarehe 13 Januari, 1978. Viongozi walioshiriki kutia saini makubaliano hayo walikuwa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Ndugu Benjamin William Mkapa na mwenzake Ndugu Joaquim Alberto Chissano wa Msumbiji.

Chuo hicho kilitoa mafunzo si kwa askari wa Msumbiji tu bali nchi nyingine kama vile Angola, Zimbabwe, Namibia na Afrika Kusini ambapo mafunzo ya utawala na uongozi wa kimkakati yalitolewa ili kuzijenga upya nchi hizo baada ya kuwa huru. Chuo hicho kwa sasa kinajulikana  kama Chuo cha Diplomasia.

SADCC

Baada ya nchi zilizokuwa Mstari wa Mbele kupata uhuru, Tanzania iliendelea kushirikiana nazo na kuanzisha Jukwaa la Uratibu wa Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADCC) mwaka 1980 ili kukabiliana na changamoto zilizotokana na utawala wa kikoloni na ubaguzi wa rangi. Mnamo mwaka 1992 Jukwaa hilo lilibadilishwa na kuwa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ili liweze kukabiliana na changamoto mpya za kiusalama zikiwamo umaskini, rushwa na matatizo yatokanayo na chaguzi.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!