NJUGUMAWE
KWA KIINGLISHI ZINAITWAJE!?
Nakumbuka
Mara ya Mwisho Kuzitia Kinywani Ilikuwa ni Zaidi ya Miongo Mitatu na Nusu
Iliyopita Tukiwa Mandarini.
Porojo na
Ndarire bila Ndaro za Fikra Nasaha
Njugumawe zile
zilivuta tamaa na Ghamu, iliyoletwa na njaa pamoja na Raghba tulizokuwa nazo
kutwa nzima, zilikuwa zimeungwa kwa tui la nazi ya Mdondoo, zikaongezewa ladha
ya Iliki kidogo na kwa sukari ya Kurashia.
Tukiwa kwenye
Marago, huku tumekaa juu ya jamvi lililoshonwa kwa Mafunjo, tukikingwa jua na
Shamiana. Sariri zikiwa zimening'inizwa huku na kule. Angani mwonzi wa jua
ulikuwa umefichwa na Moshi wa Mafunde funde.
Kweli
Nikaginizika kuwa "Mzungu wa kula hafundishwi mwana," maana chakula
kile jinsi kilivyokuwa kitamu, kiasi cha kuwavutia Sisimizi, wakija kwa Mdorongo,
wakiokoteza vilivyo dondoka ardhini.
Pembeni juu
kidogo, kuna Shubaka kubwa, kumewekwa Runinga ikionyesha kipindi cha ngoma za
asili, na wacheza ngoma ya Mdurenge wakicheza kwa namna ya Mdomwa.
Mandharinyuma, ilikuwa
ni ya milima na mabonde kwa mbele ilikuwa uwanda mpana wa Nyika bulibuli. Juu
angani, Vijumbamsale, Vinega na ndege wengine wakiruka kwa amani.
Nyuki, Bunzi, vipepeo
na wadudu wengine wakiruka kujitafutia riziki huku na kule, wengine wakimkimbia
Chekeamwezi, kiasi cha kuifanya mioyo yetu kuwa na Buraha na furaha.
Upepo mwanana Pepezi
ukipiga nyuso zetu, ukituburudisha, na kufanya Chamchela ndogo ndogo za hapa na
pale.
Nyani Wakiriarilika
huku na kule, wakituonyesha Ngoko zao. Juu ya miti kulikuwa na Kindi
wakikimbizana na Goromwe na kwa mbali tukiwaona Ngosi, Dondoro, Funo, Pundamwitu
na Hayawani wengine wakila nyasi mbugani na wengine wakinywa maji bwawani, wakiwemo
pamoja na Kongoti.
Upande wa pili
wa Jimbu, tukiwaona Twiga kwa madaha, wakikimbizana, tukinogeshwa sana na
Milonjo yao, kiasi cha kuwaduwaza baadhi yetu, ilikuwa mandhari yenye kupendeza
na kuvutia, ikituonyesha utukufu wa Muumba, katika uumbaji wake.
Pembeni yangu
kulikuwa na Konzo pamoja na kisu cha Msasi. Ndani ya Shamiana kwa juu, kulikuwa
na Visusu kadhaa, vilivyotawanywa huku na kule.
Tukiwa
tumehamanikishwa na mlo, Ghafula mvua ikaanza kunyesha, na kupelekea majani ya
Mnyegea ulioko karibu, kudondosha matone makubwa ya maji, kiasi cha kutengeza
Mvo na huku Riha ya vumbi la udongo ikahinikiza eneo zima.
Sauti ya Mungurumo
mkubwa wa Radi ikasikika angani na kuifanya mioyo yetu kushituka, huku
ikitanguliwa na mng'aro mkali wa umeme...
Nikanyanyua
Rununu yangu na kuangalia muda, ilikuwa ni saa kumi na moja unusu za jioni,
nikakumbuka jambo lililonifanya nitabasamu, nikajiuliza tena…
0 comments:
Post a Comment
Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?