PIRIKAPIRIKA ZANGU
Baada ya Maghribi, Mitaa ya Kariakoo
Nipo jijini
Daresalama, vitongoji vya mitaa ya Kariakoo, unyounyo na rafiki yangu,
tukitembea sako kwa bako, hamadi kibindoni tukajikuta tupo mtaa ya Msimbazi,
kona na mtaa wa Magila.
Kwenye kijiwe
hiki cha Kahawa, kumekusanyika wazee kwa vijana wapo himahima kama wapo kwenye
Matwana, wakiongelea matokeo ya mpira kati yao na watani zao wa jadi. Aghlabu
mazungumzo haya hutokana na ile hali ya kutamaukiwa na tamaa ya kupata ushindi
tu.
Nikasimamisha
masikio kama Sungura aliyona mbwa wa Msasi, nipo angeange kusikiliza, sina
ngoma sina maulidi, nasikiliza kinachojiri kwenye mpororo wa majaka ya
majadiliano yale, wakiongelea makorowezo ya kile kilichojiri kabla...
Nikawasikia
wakiongea kwa raghba, huku mzee mmoja wa makamu akitikisa bakora yake ya
mkanja, akisema kwa hamaki kabisa; "...hii kamati ya ufundi ni bure
kabisa, hivi wameshindwa nini kumtupia Kibuki yule sijui anaitwa nani yule,
Mayenu sijui Mayele? Jini mmoja tu toka Komoro, wa kumpindisha kidole gumba cha
mguu, ashindwe kupiga mpira. Na bado wanajiita wachawi, mbona..."
Mwingine
akadakia; "Wanashangaza sana... yaani ovyoo kabisa"
Huyu mwingine
naye akiwa na miraa na huku mashavu yake yametuna kama anauguwa Matukwa; Weee!
Unafanya mchezo na Wangwana, Mkongo yule, hakuna anae weza kumjaribu..."
Mwingine
akaingila kati: Bongo kuna Wachawi!? Wao kazi kusumbua watu tu, usiku kwenye
mapaa ya nyumba, harafu kwenye ishu za muhimu hawaonekani!
Mwingine
akamuunga mkono kwa kusema; "...umeonaa eeh usiku kwaruuuu kwaruuuu kazi
za muhimu hawazioni, yaani yule jamaa kasababisha baba mkwe kalazwa sipitali,
kwa presha, yaani waganga wa Bongo ovyo kabisa..."
Na huyu
akarukia; Sasa sijui kama ni waongo au wanazidiwa mbinu hapo ndo hatujajua...
Bwana weee! Bongo
kuna wachawi, wachawi wa Tanzania wana uchawi wa kuroga ndugu zao tu...!
Yule mzee
aliyekamata bakora yake ya mkanja, akaongeza kwa kusema; "Kwanza huyu
Mayele, anapaswa kushtakiwa, we uoni zile nywele zake kama vitunguu saumu,
wazee wengi wanateswa na mengi kuhusiana na huyu kijana, sipitali zimejaa
wagonjwa wa presha kwa ajili yake, tukimwachia anaweza kutuletea inalilahi hapa
nchini, watoto zetu tukawaacha mayatima na wake zetu wakawa wajane..."
Sauti ikasikika
toka nyuma; "Akamatwe kwa kweli na vinywele vyake kama dudu washa, kwanza
kuweka nywele vile ni kinyume cha haki za binadamu..."
Akadakia
mwingine; "Huyu sisi hatuendi kumfungulia mashtaka wala nini, tutamshtakia
kwa Mungu tu, matokeo yake atayaona, albadiri moja tu ya mtama mkavu na yai
viza vinamtosha, hawezi kutunyima raha..."
Sauti moja
ndogo ikasikika; "Wallahi tusipokufa mwaka huu, hatufi milele nakwambia,
si kwa mateso haya, kudadeki, hii nchi ngumu sana... Shubaa miti huyu laanakum
chura pori huyu, mbinguni aendi huyu..."
Mwingine naye;
"Yaani we acha tu, tumekuwa kama mwanamke aliyepaka liwa, iliyofumaniwa na
mvua...!"
Mmoja akasema;
"Tatizo sio Simba wala Mayele, tatizo Katiba ya nchi yetu, maana sheria ya
nchi inaruhusu Simba kufungwa mara kwa mara, tukibadirisha katiba, hatutafungwa
tena...."
Mmoja akauliza;
"Hivi kweli mashabiki wa Dar mmeshindwa kweli kumtafutia jishangazi hapo
Magomeni au kule Tandale kweli, jishangazi la haja, limtulize Mayele, kwani
yule Ashura wa Tabata ni shabiki wa timu gani, hivi kweli ameshindwa kumteka
nyara ile siku, leo ingekuwa raha mustarehe hapa!"
Na huyu naye;
"Kwanza alicho kifanya Mayele jana kweli hakikubariki kabisa kwenye sheria
za Fifa, yaani anamsindikiza mwenzie kwa kutetema daaaah!"
Kijana mmoja
naye akachangia; "Tatizo huyu mzungu ni wa royo tua, kacheza danadana basi
wakaona anaweza, wakamleta... Ila nasikia ni ajenti wa vifaa vya sensa!"
Sauti ikasikika
ya jamaa mwingine, kidogo tende ilikuwa ishamkolea kichwani, akiongea kwa
kigugumizi; "Hu-hu-huyu jjjamaa Ma-ma-ma-mayele si-si-sisio ji-ji-jina
la-la-lake na-na-na ndo ma-ma-maana wa-wa-waki-ki-kiroga ji-ji-jina la
Ma-ma-mayele ha-hapatikani na-na-na ji-ji-jina la-la-lake ni-ni-ninge-ninge
wa-wa-tajia i-i-ila ta-ta-tati-titi-zo
ha-ha-ham-m-mni-ni-nisa-sa-sali-li-limiagi...!"
Mmoja
akakumbushia; Mie nawaambia, ile ni laana ya kwenda na mthalaba na jeneza
kwenye thimba dei, ndio maana mthimu wote hu tutashindwa tu. tumewakathirisha
midhimu ya mababu..."
Ghafla Swahiba
wangu akanigusa bega, kaka unasikia adhana hiyoo, isha ishaingia, twende tukawahi
hapo Msikiti wa Idrissa... Tukaongozana kuelekea kwenye kufaridhika...
MSAMIATI
WA MANENO MAGUMU
- 1. Angeange:
Kuonyesha umakini au utayari wa mtu au kitu
- 2. Kibuki:
Aina ya Majini
- 3. Kufaridhika:
Kulazimika, Ulazima, wajibu
- 4. Kutamaukiwa,
Tamauka: Kutokuwa na tamaa au matarajio ya kupata kitu. Kata tamaa
- 5. Liwa:
Rojo ya mliwa na sandali inayotumika kuwa ni manukato au dawa ya joto la Ngozi.
- 6. Majaka:
Pasipo kufuata utaratibu uliowekwa.
- 7. Makorowezo:
Hali ya kuchanganyikiwa, hususani katika kufanya jambo fulani.
- 8. Matukwa
au Matukwi: Ugonjwa wa kuvimba mashavu.
- 9. Matwana:
Lori au basi la kubeba abiria Pamoja na mizigo yako mf: Chai Maharage
- 10. Miraa:
Mirungi
- 11. Mkanja:
Mti unaomea porini na kutoa fimbo ndefu na nyembamba
- 12. Mpororo:
Mfuatano wa vitu au watu.
- 13. Msasi:
Mwindaji wa wanyamapori.
- 14. Raghba:
Hamu inayomfanya mtu atende jambo fulani, muhemko, shauku, haja.
- 15. Sako
kwa bako/Sago kwa Bako: Andamana au tembea pamoja ubavu kwa ubavu
- 16. Sina
ngoma sina maulidi: Kutofurahia jambo
- 17. Unyounyo,
Unyo: Kufuatana Pamoja kwa nyuma, andamana.
- 18. Wangwana:
Waswahili wa Kongo
0 comments:
Post a Comment
Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?