JIJI
LA DAR US SALAAMA
DAR ES SALAAM TANZANIA
Kabla ya mwaka 1868, Jiji
linalofahamika kwa jina la Dar es Salaam, halikuwepo kabisa. Badala yake
kulikuwa na mji ulioundwa na miji mitatu maarufu, ambayo ni Kunduchi, Mbwamaji
na Tindwa. Kila mji ulijitegemea, huku idadi ya wakazi wake wote kwa jumla
haikuzidi watu 2,000.
Kati ya miji hiyo mitatu, miji
miwili ya Kunduchi na Mbwamaji bado ipo hadi leo huku mji wa Tindwa, uliokuwa
na eneo kubwa zaidi, ulimezwa na nguvu za matukio ya kihistoria
yaliyosababishwa na mabadiliko na mpangilio mji mzima wa jiji.
Tukio kubwa la kihistoria
lililobadili mpangilio wa miji hiyo mitatu na kuzaliwa kwa Jiji ambalo leo hii
linalofahamika kama Dar es Salaam lilitokea mwaka 1865 pale Sultani Majid,
aliyekuwa mtawala wa Zanzibar, kununua eneo kubwa la ardhi ya mji wa Tindwa,
iliyomilikiwa na Sharif abdushakur Salim Al Attas na Jumbe Tambaza (machifu wa Kimashomvi), eneo
hilo lilianzia Bustani ya Mnazi Mmoja karibu na Mnara wa Saa (Clock Tower)
mpaka Magogoni (Ferri) mpaka kuelekea Daraja la Selender kutokezea Upanga
lilikuwa ni Shamba la Jumbe Tambaza.
Lengo la Sultani huyo la kununua
ardhi hiyo inayoanzia eneo la Magogoni hadi eneo la Hospitali ya Osheni Rodi
(Ocean Road), eneo ambalo lilikuwa pori linalotazama Bahari ya Hindi na ambalo
lilikuwa na ukimya, kiasi cha wakazi wa eneo la Tindwa kulipa jina la Mzizima,
kwa sababu kila aliyepita eneo hilo alihisi mwili wake kusisimka na kuzizima
kwa hofu ya kuwaogopa Wanyama pori.
Alinunua hilo eneo na kujenga
majengo makubwa kwa ajili ya kufungua chuo/shule ya kufundisha dini ya Kiislamu
kwa lengo la kueneza Uislamu kutokea hapo kuelekea maeneo mengine ya Mrima,
Pwani na Bara hadi Kongo na Burundi na kwa watu wa nchi za ukanda wa Afrika
Mashariki, Afrika ya Kusini na Afrika ya Kati.
Baada ya kununua eneo hilo, mwaka
1865 Sultani Majid aliingiza manuari kubwa za mizigo, zinazokadiriwa kuwa kati
ya tatu hadi saba, zikiwa zimesheheni vifaa vya ujenzi na wataalamu wa ujenzi
wa majengo ya chokaa na mawe, toka nchi za Bara Hindi na Uajemi. Na ndipo
ujenzi wa majengo hayo ulipoanza kwenye eneo hilo la Mzizima mkabala na pwani
ya Magogoni, huku majengo mengi yakijengwa eneo la Ocean Road.
Pamoja na Ikulu ile ya Magogoni,
Seyyid Majid pia alijenga lile jumba la ‘Ocean Road Cancer Institute’ (ORCI)
kwa sasa, ambalo mwanzoni lilikuwa ni Msikiti Mkubwa wa Ijumaa.
Ujenzi wa majengo hayo ulichukua
takribani miaka mitatu na kukamilika mwaka 1868 na Sultani Majid mwenyewe
alilipa jengo moja kubwa lilipo Magogoni hadi leo, jina la Dar us Salaama
(tamka Daru Salaam), maneno ya Kiarabu yenye maana ya Nyumba ya Utulivu au
Nyumba ya Amani. Na katika lango kuu pameandikwa maneno kutoka kwenye Qur’an
Suuratul Hijr Ayah ya 46 isemayo (ٱدْخُلُوهَا بِسَلَـٰمٍ ءَامِنِينَ)
Udkhuluuhaa Bisalaamin Aaminiin (Ingieni kwa salama na amani).
Wakoloni wa Kizungu walipokuja
Tanganyika, mahala hapo ambapo palikuwa ni Msikiti Mkubwa wa Ijumaa, pakafanywa
hospitali iliyojulikana kama ‘Ocean Road European Hospital’, iliyokuwa
ikiwatibia Wazungu peke yao.
Na ndio utaona vijana wengi jiji
la Dar es Salaam waliozaliwa baada ya uhuru kati ya miaka ya 60 - 70,
wamezaliwa kwenye hospitali ya Ocean Road, ambayo sasa ni maalum wa kutibu
saratani (Ocean Road Cancer Hospital), na kabla ya hapo yalikuwa ni majengo ya
msikiti na mabweni ya vijana na wazee waliokuja kusoma Dar Us Salaam na bado
mpaka leo muonekano wake ni ule ule.
Ikulu ile ya Magogoni wakati huo,
ilikuwa imezungukwa na misikiti kadhaa ambayo yote, katika Utawala wa
Kijarumani, ilibadilishwa matumizi na kufanywa taasisi nyengine.
Misikiti mingine iliyobaki
ikasambaratishwa na kutumiwa kwa shughuli nyengine, ukiwamo Msikiti mkubwa
uliokuwa baharini pale Forodhani, jijini Dar es Salaam, ulipogeuzwa kutoka
msikiti na kuwa Kanisa la Mtakatifu Joseph mpaka hivi leo.
Kuanzia hapo, wakazi wote wa miji
mitatu ya Kunduchi, Mbwamaji na Tindwa, wakabadili jina la Mji wa Tindwa na
kuubatiza jina la jumba hilo kubwa kuwa Dar us Salaama, jina ambalo baadae
lilimeza hata majina ya miji ya Kunduchi na Mbwamaji na kuifanya iwe vitongoji
tu katika mji wa Dar us Salaam.
Kwa takribani miaka kumi tangu
kufunguliwa kwa jengo hilo, raia toka nchi mbalimbali kuanzia Tanganyika,
Msumbiji, Zaire, Burundi, Rwanda, Kenya na Uganda, walimiminika katika jumba
hilo na kupata elimu ya Uislamu iliyotolewa na masheikh wakubwa toka nchi za
Uarabuni, Lamu na Mombasa Kenya na Zanzibar.
Kati ya mwaka 1875 na 1878,
Wajerumani walivamia Tanganyika na kuiweka katika himaya ya utawala wao, na
jengo hilo lilibadilishwa matumizi yake toka kuwa kitivo cha elimu ya Kiislamu
na kuwa makao makuu ya serikali ya Kijerumani na baadae kuwa makazi ya Mtawala
wa Kiingereza na leo hii ni Ikulu ya Taifa.
Mbali ya kubadilishwa jina kwa
jengo hilo, toka Dar ul Salaam na kuwa Ikulu, hata jina lilipewa mji wake
kutokana na jengo hilo pia limebadilishwa toka Dar us Salaama (Nyumba ya
Utulivu/Amani) na kuwa Dar es Salaam (Bandari ya Amani) ambayo wajuzi wa lugha
ya Kiarabu wanakata kuwa neno hilo Dar es Salaam halina maana ya Bandari ya
Salama.
NB:
Maelezo Kutoka kwa Mjuu wa Sharif Abdushakur Salim Al Attas
Sharif Abdushakur Salim Al Attas hakuuza eneo lake la Shamba lake tokea Clock Tower mpaka Magogoni, sababu Sharif Attas hakuwa na watoto zaidi ya mdogo wake sharif Omar Al attas aliezikwa uani ndani ya Msikiti wa Kitumbini, na sababu ya Wajerumani (Deutsch-Ostafrika) kupora Shamba la sharif abdushakur Salim, walisema Shamba la diwani wao ndio sababu wakapora na alieuza eneo ni Tambaza.
0 comments:
Post a Comment
Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?