Friday 11 November 2022

 BIRIKA BATI, KIKOMBE BATI,
NA HATUKUKOMA.

Hivi wakulaumiwa walikuwa watengenezaji au wanunuaji au watumiaji!?

Yaani hata sielewi, vikombe gani vinaunguza namna ile? Au walikuwa wanatukomesha tukivunja vikombe vya udongo!?

Halafu kikombe cha chai, ila kinapicha ya nyanya. Sikuvipenda, sivipendi, sitavipenda.

Na kwa nini nivipende, uwenda hivi vikombe ndio vimetukomaza midomo tukiwa bado makinda.

Nahisi ndio maana Watanzania tumekuwa watu wa kupiga sana stori... Sasa wewe fikiria chai ya moto, kuiwacha huwezi, hapo sasa ni stori tu, kumbe janja yako unavizia ipowe, hapo ni stori plus umbea na mikingamo.

Basi nikwambie, siku hiyo nikamtembelea binamu yangu wa kike maeneo ya Magomeni, nikitokea zangu maeneo ya Gerezani, Kariakoo, chini nimevalia viatu vyangu vya Kung Fu shuzi, medini Chaina. Shati langu la Juliana, picha ya ndege, kubwa kiasi na chini nimevalia suruali yangu ya kodrai.

Mtu mimi na ufupi huu, ukiniona kwa mbali, utafikiria nguo zatembea zenyewe. Huyoo kiguu na njia, nikakatiza zangu Jangwani, na jua lile la saa tisa alasili. Kufika home kwake, kanikaribisha uwani, nyumba nzima yupo peke yake, wapangaji wapo mitaani, awajarudi bado.

Kanikaribisha kwenye Kigoda, baada ya salamu na kujuliana hali akanikaribisha chai ya mkandaa, akanitilia kwenye kombe la bati, chai imekolea viungo, inawasha kwa karafuu na tangawizi, ikakolezwa na pilipili mtama, chai kama uji wa mgonjwa na mie ujanja ikawa ni kupiga stori za kupoza chai, fu fu fuuu, nyiingi!

Japo tupo uwani, lakini joto la saa tisa, jiji Dar nalo halikuniwacha, utafikiri nimemwagiwa maji, mara akanyanyuka na kuniita niende chumbani kwake...!

"Binamu njoo chumbani nikuonyeshe mambo, ila nakuonya usimwambie mtu..."

Ghafla nikajikuta nameza mate machungu, nahisi nilitaka kutema nyongo, ikaishia kohoni, chai kidogo inipalie, nilajikuta naimeza bila kujua kuwa naunguza kolomeo.

Nami bila ajizi nikajikuta nipo chumbani, hata sijui nimefikaje, maana fahamu zikikuwa zinaingia na kutoka...

Hakuna pa kukaa ila kwenye kitanda, mwenyewe katandika mashuka yake ya kufuma kwa mkono, maua ya rozi (mawaridi), kafanya seti kamili, mapazia ya dirishani na mlangoni. Vingine kafunikia radio yake, kaseti aina ya National na kitambaa kingine kakitandika kwenye meza.

Pembeni ya chumba kuna mtungi wa maji, umefunikwa na sahani ya bati na kata yake imewekwa pembeni kidogo, picha za wanamuziki wa Boney M na ABBA group zilizokatwa kutoka kwenye magazeti ya Sunday News zimebandikwa ukutani, pamoja na picha ya Buraku, kafanana na mwanamke wa Kihindi.

Kwenye meza kuna viboksi viwili vitupu vya sabauni ya Lux na lifebuoy pamoja na kibox cha dawa ya kusugulia meno ya Colgate. Pembeni kidogo, kuna kabati la vyombo lenye wavu, na kabati la nguo lenye kioo.

"Kaa basi hapo we nawe wima wima tu, kama mgambo wa site" sauti yake ikakatiza mawazo yangu yaliokwenda mbali ya hapo, maana mawazo yalikuwa mbingu ya sabaaa nacheka na kufurahi na malaika wa peponi.

Nikakaa kitandani, moyo unakwenda kasi kama wa Mbayuwayu... Akanitazama kisha akanambia, huku kaweka umakini usoni, yaani yupo siriasi kabisa... "binamu hii iwe siri yetu, ukimwambia mtu, mi na wewe basi tena sitakushirikisha kwenye mambo mazuri haya."

Nikahisi masikio ghafla yamenisimama wima kama mbwa wa msasi kaona windo, nikanyoosha na shingo kama Njiwa Manga...

 Nikahitikia kwa kutingisha kichwa, akanambia "Apiya binamu, kuwa hutotoa siri, sema Hakiyamngu..." nikajikuta natamka, kwa kigugumizi, kilicho nikamata, hata kilipotokea sijui...

"Ha-ki ya M-ngu tttena, si-si-mwambii m-mtu mi mi-ye, Waalaahi Nakuapia, mmmh na mchanga huu naramba." Huku nikiinama na kwa kutumia kidole cha shahada, nikapangusa sakafu na kuramba...

Moyo ukaongeza kasi kama garimoshi la Mjerumani kwenye vita kuu ya kwanza ya dunia sanjari na tumbo likapata kusema, gruuuh.

Akanitazama kisha akanambia: "Haya mie nakuamini voo binamu yangu, najuwa we mambo yako ya kizungu, ndio mana nakupendaga..." Akatamka huku anaelekea kabatini kwake na kufungua kabati...

Hamadi, katoa doti tatu za vitenge vya wax na kuvirembea pale nilipo kaa, kitandani. Enzi hizo tukuvihita vitenge vya Burundi.

"Nimeletewa jana na shemejio..." Sauti yake ikaanikiza pale chumbani.

Nikamuuliza, Mmm! Shemeji yupi huyo...!? Yule mjeshi wa Ngerengere!?

Akanijibu: "Uwachi na wewe, wa Ngerengere wapi!? Yule nishamtosa siku nyingi... Huyu humjuhi wewe, mwenyewe anafanyakazi bandarini, hivyo vitenge vya Magamu (Magendo), vilikuwa vinapelekwa Burundi kontena nzima, yeye ndio kavinyakua hivi vitatu, kaniletea nimuuzie."

"Kimoja shilingi 25, ila kwa wewe binamu yangu, nitakuuzia kwa shilingi 22, na wewe ukauze upate faida japo kidogo."

Nikamtazama, kisha nikapiga fundo moja la chai ya moto, yaani hata sikuhisi kuunguzwa, hiyo midomo na koromeo nilikuja kuhisi nimebabuka, usiku wake nisharudi nyumbani.

Ghafla nikajihisi kama biskuti ndani ya chai ya moto au kiowevu, nikawaza mfukoni nina shilingi Moja ya Mwenge na sumni tu ile ya sungura...

Enewi, yalikuwa tu maisha yenye changamoto zake, furaha, uzuni, vicheko vyote vilikamilisha uhalisia wa maisha yetu, hatukuacha kutembeleana, japo bidhaa muhimu zilikuwa adimu... kula kwa kaya...


😉🤭🤣

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!