Tuesday 8 November 2022

LIKIZO YANGU, JIJINI DSM (DIZIM)

Na Kumbukumbu Iliyopotea

Nilipokuwa likizo jijini Dar es salaam, nikajikuta tu nimepata hamu ya katembelea kwa miguu, mitaa ya Gerezani, Kariakoo. Nikapitapita mitaa iliyosongamana watu wa kila aina, nikakumbuka kufuchama Rununu yangu, kwa kuchelea wivi, wasijeichukua bila ruhusa yangu, huku sauti za wabeba mizigo wakiyosayosa maneno ya kutiana nguvu, nikapishana na wenyeji wachache sana, wakihisabika kwa vidole vya mkono, wengi wao ni wageni.

Huyo nikayoyomeka zangu, nikajikuta natokea mtaa wa Nkrumah, taratibu nikashuka zangu mwelekeo wa Mnara wa saa, nikatupa macho upande wa kushoto nikasoma kibao, kilichofubaa kwa rangi baada ya kutelekezwa miaka dahari, neno NEW CHOX bado likisomeka, kumbukumbu ikarejea miaka mingi nyuma, nikatabasamu sanjari na kusikitika, maana umuhimu wa jengo hilo kwa sasa haupo tena, nani anakwenda sinema siku hizi!?

Hata ile hoteli ya Continental sina uhakika kama bado inatoa huduma, nakumbuka tulikuwa tukienda kucheza Disco na vijana wenzangu.

Nikakumbuka hata wale wakaazi wa vitongojini, nao hawakuachwa nyuma, serikali iliwafungulia vituo vya burudani vya kijamii, kwa wakazi wa jiji la Dar, watakuwa wanakumbuka majumba ya DDC, kama vile Amana Social Hall, DDC Kariakoo, Keko na pale Magomeni.

Pale Ilala awali ilikuwa pia ni mahali ambapo wengi wakienda kungalia sinema siku za mwisho wa wiki na siku za sikukuu. Kiufupi majumba haya ya jamii, yalikuwa nchi nzima.

Nikakumbuka kuna jumba moja lilikuja mwishoni, katika miaka ya 80, jumba ambalo ndio lilikuwa jumba lenye uwezo wa kuingiza watu wengi sana, likijulikana kwa jina la Star Light Cinema.

Kiukweli hii ni kumbukumbu nzuri na ya kuuzunisha, maana enzi hizo kweli ilikuwa jambo la tunu sana kwa mtoto au hata mtu mzima kupelekwa sinema.

Kwanza halikuwa jambo rahisi kwa mtu tu asiye na ubavu kupata tiketi, haswa filamu ikiwa ni mpya na waigizaji wakiwa ni maarufu.

Nakumbuka walanguzi wa tikiti za sinema, vijana kwa watu wazima, wenye nguvu zao, wengi wao weshatangulia mbele za haki, walikuwa wakimaliza kulangua pale New Chox sinema, walikuwa wakikimbilia Avalon sinema, alafu sasa pale kidirishani, tikiti zilikuwa zikiuzwa nusu, kisha zilizobakia wale Wahindi wakiwapa watu wao na kuziuza kwa bei ya juu.

Nikajikuta natabasamu, kumbukumbu iliyokuja baada ya hapo, nikatamani kucheka, maana siku hiyo pale Chox niliwahi kidirishani kabla ya dirisha la kununulia tikiti halijafunguliwa, nikajuwa leo napata tikiti tena zile siti za nyuma kabisa, kama si mstari A basi D.

Ghafla lango likafunguliwa kuruhusu watu waingie kununua tikikiti, sanjari na dirisha la kuuzia tikiti, hamadi nikajikuta hewani kama Sapatu, nimepigwa kibega kimoja tu, nikajikuta nimetupwa huko karibia na vyoo, chali kama mtoto wa Komba kaanguka mtini.

Nikajizoazoa zangu, nikabakia nimetumbua zangu macho kama mtu aliyekabwa na nguto, kumeza siwezi wala kutema ziwezi. 

Enewei, pale jumba la sinema la Empire nako wakimaliza kuuza, walikuwa wakienda zao Empress, Ila jumba ambalo vijana wengi wakilipenda ni jumba la Empire kwa sababu walikuwa wakionyesha sinema nyingi za hollywood, na waendeshaji walikuwa na tabia ya kuongeza sauti haswa wakati wa mapigano, ili kuwakoleza watizamaji.

Majumba ya Cameo (Mtaa wa Jamhuri,) na Odeon (Mtaa wa Zaramo na Jamhuri) haswa yalikuwa maarufu kwa sinema za Kihindi, wakifuatiwa na New Chox Cinema (Mtaa wa Nkuruma) na Avalon (Mtaa wa Zanaki) na Empress (Mtaa wa Samora) alafu ndio Empire (Mtaa wa Azikiwe). 

Kule Msasani, kulikuwa na jumba la sinema, likitwa Drive-Inn, wakiingia na magari yao, ila wakazi wa Msasani wengi walikuwa wakijazana nje ya ukuta na kutazama sinema, japokuwa hawakuweza kusikia sauti lakini wengi wakiridhika na hiyo hali.

Drive-Inn-Cinema
Drive-Inn Cinema

Nakumbuka kumtembelea Marehemu, ndugu yake na baba, mitaa ya Msasani, sasa ndugu yangu mmoja (yeye ni mkubwa kuliko mimi, naye pia ni marehemu), akanipa ofa bubu ya kwenda kutazama sinema, ah ah ah ah, akanipeleka Drive inn, kufika tukakaa nje ya ukuta na kununu zetu karanga na maji ya sharubati, tukatafuta tofali na box chakavu kisha tukaa kuangalia movie, tukisumbuliwa na mbu hapa na pale.

Sikumwambia kitu maana nilikuwa nikimuheshimu, mwenyewe nilishazoe kwenye majumba yetu ya kawaida, kama ukishindwa kununua tikiti basi unafanya kila njia kupenya au unampa pesa kidogo mwangalizi wa tikiti na kukuingiza ndani, ila kama jumba limejaa, basi unakaa kwenye ngazi za kutokea nje... Ah ah ah ah, ama kweli siku hazigandi.

Vijana wa leo wanaweza kushangaa wakisikia kuwa hata wimbo wa Taifa ulikuwa ukipigwa kabla ya onyesho, ila baadae sana ikaja kuondolewa kwa sababu ilisemekana kuwa hakukuwa na heshima, sababu wengine walikuwa ni walevi na hawakuwa wakisimama wima pale wimbo wa Taifa unapopigwa.

Hii biashara ya sinema ilikuja kuanza kudorora vilipoanza vituo vya Runinga na kushamili kwa biashara ya kuazimana kanda za video, na maktaba za kukodisha kanda za video, hizo zilikuwa enzi za Mzee Ruhsa. 

Wengi walikuja kupendelea kukodisha kanda za video kuliko kwenda kwenye majumba ya sinema kwa sababu kwanza ilikuwa ghali kwa mtu mwenye familia, kugharamia watu zaidi ya wanne, pili filamu zenyewe nyingi zilikuwa baadae zikirudiwa rudiwa, nadhani shirika la filamu Tanzania lilikuja kufirisika na kushindwa tena kuagiza filamu mpya.

Haya majumba ya sinema, siku za mwisho mwisho walikuwa wakionyesha filamu mbili mpaka tatu kwa malipo ya kutazama filam moja, yaani ilikuwa ni kukesha, maana zilikuwa zikianza usiku.

Nakumbuka filam moja ya kihindi ilitamba sana katikati ya miaka ya 70 na mwanzoni mwa miaka ya 80, filam yenyewe ilitoka mwaka 1975. Ilitwa Sholay, hii filam Wahindi wa bongo walichapisha mpaka fulana zake na kuziuza!

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!