Monday, 5 December 2022

 NILIKWENDA KUNUNUA MWENYEWE DUKANI

Hivi Siku Hizi Bado Kuna Wanao Tafuna Tambuu!?

Nipo Zangu Likizo, Ndani ya Jijila la Dar, Nakatiza Mitaa ya 'Uhindini' Karibu na Palipokuwa na Jumba la Sinema la Cameo, Lengo ni Kuelekea Walipokuwa Wakiishi Wakwe Zangu, Mtaa ya Kisutu.

Nikaikumbuka hii mitaa enzi hizo nikiishi mtaa wa Livingstone, walikuwa wakiuza sana Tambuu, ila ni ayami sasa sijaona 'Wahindi' wala 'Waswahili' wakitafuna Tambuu.

Zamani ukipita hii mitaa unakuta watu wanatafuna tu. Sasa usiombe jamaa awe anatafuna akiwa ghorofani halafu 'aipunguze' mdomoni wakati wewe unapita chini. Utasimulia.

Nikakumbuka kisa kilichonipata, miaka kadhaa nyuma. Nipo zangu nyumbani, mtaa wa Livingstone, Kariakoo. Miaka ile ya 80, bado kinda hata ubwabwa wa shingo bado kunitoka, sina hili wala lile. Hata sijui lile wazo lilikuja vipi, ila mpaka leo naamini kabisa, yaani haki ya Mungu tena, ndani ya mtima wangu kuwa; siku ile nilitembelewa na ibilisi wa Kibaniyani.

Tena atakuwa ni Mgujarati tu afiriti yule ayari, maana si kwa ushawishi ule ulionikamata, kiasi cha kushindwa kufikiria vizuri. Wala sikuwa na uraibu wa kula Tambuu, ila siku ile nilikamatika, nikajikuta nipo kiguu na njia kuelekea maeneo ya Kisutu, Uhindini.

Nikakatiza zangu Mnazi Mmoja, huyoo kiguu na njia, nikapita Mtaa wa Libya, mpaka makutano ya mtaa wa Libya na Zanaki, kisha nikachepuka kidogo kuingia mtaa wa Mtendeni, kisha nikaingia mtaa wa Mlima, kabla ya kukanyaga mtaa niliokusudia, mtaa wa Kisutu, dukani kwa Muhindi, Makaputura.

Ni baba wa Makamu, mnene haswa, kakaa dukani kwake, akipenda kuvaa kaputura akiishikiza kwa anjali, na ndio ikawa rakabu yake, Mzee/Babu Makaputura. 

Duka limesheheni vitu kadhaa wa kadha, vimewekwa bila mpangilio maalum. Harufu ya Agarbatti inachomeka iliyowashwa mbele ya Ganesha na Lakshmiina, ina hanikiza kiasi cha kukera kwenye pua, harufu badala ya kuanisi ikawa inakera kiasi.

Akanitazama, bila ya kutabasamu, anafungua kinywa chake kunisemesha, huku nikishuhudia meno yake, yaliyobadirika rangi na kupata rangi ya Kahawia, iliyochanganyika na Chanikiwiti na mdomo wake uliojaa mate Mekundu kama damu kwa kula tambuu.

Kisha anatema mate mekundu yasiyopendeza, "Nini nataka veve", akaniuliza kwa rafidhi yake ya Kihindi, nami nikajikuta namjibu bila kufikiria, nataka tambuu, akanitazama kisha akaniuliza, "Nani Natuma veve tambuu" Kaka, nikamjibu, "Nambari gani iko nataka" nikamjibu, namba kumi na tatu, "Nambari Kumi na tatu, Taveja yeye" ndio babu, we nipe tu, ataiweza, nikamjibu. "Nataka gapi, bili, tatu inne" Moja tu inatosha.

"Haya subiri kidogo nategeza wewe, ile spesho kabisa, Tikee" uku akitingisha kichwa chake... Nikaitikia Tikee. Kulikuwa na majani ya Tambuu mezani, akachukua jani moja akalipangusa kidogo, kisha akaweka Popoo pamoja na chokaa kidogo juu ya jani la mtambuu, akaongeza na Tumbaku, Kungu Manga kidogo, Jagir gur na vikorokoro vingine wala sivikumbuki tena.

Akachana gazeti na kunifungia, "haya lete shiligi bili", nikampatia, kisha huyoo nikaongoza kurudi zangu, nyumbani. Nikapita mtaa wa Mrima, nikafungua kifurushi changu cha tambuu, nikabugia yote kinywani.

Sikumbuki kutema mate, kila yakijaa kinywani, nayameza kwa ule utamu wa ile sukari guru... Dakika si nyingi, nikaanza kuhisi Andasa ikipanda kidogo kidogo.

Afanaleki! Nikaanza kuhisi ubongo wangu haujatulia, harabu ya ile tambuu, yaani chugachugia, nilitia akili siku hiyo, dunia yote niliona kama inakwenda upande upande, nami nikaifatisha.

Kumbe walio niona siku ile wakastaajabu, wakapatwa na mpagao, mtu mfupi mie kwa jinsi nilivyokuwa nikitembea, kama mtu mwenye milonjo, maana si kwa miondoko ile ya mikogo.

Wakaja kuniuliza, siku ya pili yake, kumbe nilivyokuwa naangaika na andasi kichwani, na mwendo nikabadirisha, nikihisi barabara zimeinamia upande mmoja wa kushoto, nami ili nisidondoke nikajikuta natembea kuinamia upande wa kuume, natembea kama mtu aliyepigwa dafurao na lori la Jay Fong la mwaka 74.

Nilikuwa natembea kama Kaa au Ngadu, yaani nikitembea upande upande, siku hiyo niliongea lugha zote za Kihindi, Kibengali, Kigujarati, Kitelugu, Kiurdu, mpaka Kibanyani nilikijua siku hiyo... Kudadeki.

Hata nyumbani sikumbuki nilifikaje, nilijikuta tu nimepitiliza mpaka uwani, huku nimeshika kibatari nilichokiwasha, tena ni saa kumi jioni, mie naona giza.

Siku hiyo nilitapika mpaka nyongo... Nikanyororeka kama Kinyonga aliyelishwa ugoro... 

Kuanzia siku hiyo nilikoma, sikutia mdomoni si Tambuu wala Kubeli au nduguye Pariki...

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!