MBIOMBIO NIKAJIKUTA NALIKIMBILIA GARI LA KUZOA TAKA
Nilikutana Naye Kwa Kinyozi... Akauliza, Kwa Unyenyekevu Kabisa..!
Basi bhana, Nipo Zangu Varandani, Mida ya Saa Tatu Hivi ya Asubuhi, Ghafala Huko Nje Nikasikia mlio wa Gari ya Kuzoa Takataka. Nikakumbuka Kuwa Nilipaswa Kutoa Pipa la Taka Tangia Jana Usiku... Nikakurupuka kama Swala aliyekoswa koswa na Simba.
Mbiombio nikapitiza uwani, nikakutana na rasharasha za mvua, uku nikijikwaa kizingitini, sikujali sana, nikakamata kishikio cha pipa, nakaliburuza mpaka nje.
Natoka gari lishapita, lipo takribani nyumba ya Tatu toka kwangu.
Sikukata tamaa, nikapiga mbinja, huyo mbiombio nakimbiza gari wanguwangu, kandambili imenichomoka mguuni wala sina habari, kufika ni hoi, nahema kama Mjombakaka aliyekoswa koswa kunyakuliwa na Kipungu.
Nilipo wafikia mmoja wa mzoa taka, akanambia kuwa si gari hili, wao ni wa kampuni nyingine... Nikajikuta nimechoka mara dufu.
Mbio za mita kumi na tano kama si ishirini, zilinifanya niwe hoi taabani, polepole nikajirudia zangu nyumbani, nikaokota ndara yangu iliyonichomoka wakati wa kukimbiza gari la taka, nikajigundua kumbe nimelowana...!
Nikajifuta maji, nikakaa zangu sebuleni, nikajitafakari, nikakumbuka ni siku tatu tu, tangia watu washeherekee mwaka mpya.
Nikakumbuka mengi, yaliopita kwenye maisha yangu, mtu mie niliyekuwa hodari wa mbio, leo hii mita ishirini zimenitoa kamasi...!
Mawazo yakanichukuwa, yakanipeleka siku ya mwaka mpya...
Ilikuwa baada ya kumaliza Faradhi ya salah ya insha, nimekaa na Memsapu wangu, tukiongea na kucheka na huku tukitafakari jinsi Mwaka ulivyopita. Kwa mbali tukasikia sauti za Fashfashi, huku mwanga ukimemetuka. Tukakumbuka kuwa kumbe mwaka umeisha, watu wanashereheka huko nje kwa kumaliza mwaka.
Vijana wangu wakatoka hapo nje, kuangalia fashfashi, zikimemetuka angani. Dakika hazikwisha, nikakatizwa na mlio wa simu ya mkononi. Triiii! Triiii! Triiii...! Kuangali kumbe zilikuwa ni meseji zikiingia mfurulizo. Nikawa najiuliza kuna nini tena mbona meseji nyingi kiasi hiki!?
Nikaamua kuzisoma moja baada ya moja, na meseji zote zikinitakia salamu za mwaka mpya, wenye amani na maisha mema.
Nikajikuta nakumbuka kisa kimoja kilichonipata kabla ya ule mwaliko toka kwa Sahibu yangu, takribani siku sita zilizopita.
Siku hiyo nilipitia kwa Kinyozi kwa dhumuni la kupunguza kidogo nywele na kukata sharubu zangu, maana nazo zilikuwa ndefu, kama Gari Moshi la kuelekea Kigoma.
Baada ya kuchakachua mwendo nikafika kwa Kinyozi, mitaa ya Kariakoo, kumekusanyika vijana kadhaa, wapo wanaosubiri kunyolewa na wapo wenye kupiga ndaro na ndarire za hapa na pale.
Wakati nasubiri zamu yangu, macho yangu yakagongana na mzee mmoja wa makamu hivi, kakonga kiasi chake. Kumtazama vizuri na kuchakata sura yake, nikahisi kumkumbuka.
Ndio Huyu huyu, alikuwa mmoja wa vijana niliosoma nao sekondari, nikamkumbuka kijana mmoja maungo makakamavu, rangi maji ya kunde, nakumbuka nikimtania kwa jina la Andunje. Tulikuwa wote darasa moja ni zaidi ya miongo mitatu sasa imepita!
Ila sasa ndani ya nafsi yangu nilikuwa bado najiuliza, ndio huyu, kijana aliyekuwa akisumbua sana kwenye masomo ya Hisabati pamoja na yale ya sayansi!?
Nikamtazama tena na tena, hakuonyesha kunikumbuka hata kidogo nikataka kumpotezea, lakini upande mmoja wa bongo langu, likanishauri vingine. Nikatizama kichwa chake, kilichokuwa kimejaa mvi za hapa na pale, uso wake wenye makunyanzi.
Kwa jinsi alivyozeeka, asingeweza kabisa kuwa ni yule kijana niliyesoma naye darasa moja, nikajiliwaza kwa kujisemea moyoni, labda uwenda ni baba yake mdogo au ni watu tu wanarandana!
Zamu yangu ikawadia, nikajisogeza na kukalia kiti cha kinyozi, nikamuelekea jinsi gani nataka... Baada ya kumaliza na kulipa, nikapiga moyo konde na kujipa ujasiri, nikamsogelea na kumuuliza kama aliwahi kusoma shule niliyosomal?
Huku nikimkazia macho nikamuuliza, "Samahani ndungu, wewe ulisoma shule fulani hapa jijini Dasalama!?" Naye akanitazama kwa umakini bila ya kupepesa macho kisha akanijibu "Ndio, nilisoma pale..."
"Ulimaliza mwaka gani?" Nikamuuliza kwa mashaka kidogo!
Akajibu, "Mwaka 1990. Vipi kwani?" Naye akaniuliza!
Nikamakwa, "1990? Ulikuwa kwenye darasa langu!" Nikatamka, na huku mshangao wangu nikiuonyesha wazi kabisa, kwa yeye kutonikumbuka.
Akanitazama kwa muda, kama vile haamini ninachosema... Kisha sasa, Hapo ndipo nilipochoka kabisa, yaani yule babu wa watu akaniuliza, kwa unyenyekevu kabisa, "Samahani, hivi wewe ulikuwa Mwalimu wangu wa somo gani!? Maana mpaka sasa sijakukumbuka bado..."
Nikataka kumjibu kuwa mimi ni Classmate wake, ila kuna kitu kikanizuiya, akili ikafanyakazi kwa haraka sana, nikajisemea kimoyomoyo...
"Mungu wangu! Kumbe Nimechakaa Zaidi Yake, Kiasi cha Yeye Kuhisi Kuwa Miye Nilikuwa Mwalimu Wake... Nikabakia Mdomo Wazi Ukitetema, Huku Kinywani Nikihisi Tewengu, Nadhani Nyongo Ilitema Ghafla!"
Hivi Mwaka Mpya Huwa Tunasheherekea Nini Haswa, Kuzeeka!?
0 comments:
Post a Comment
Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?